MFAHAMU MWANAUME SHUJAA WA SINGIDA ALIYETUMIA MVUA KUPAMBANA NA WAJERUMANI
-Ni KITENTEMI wa Isanzu- Mkalama
-Aliweza kutengeneza mvua wakati wowote na kuituma kwa Maadui zake wajerumani na kuielekeza anavyotaka .
KITENTEMI mwanaume shujaa wa Singida aliyepambana vita kali na wajerumani walipojaribu kukanyaga ardhi ya Mkalama ambapo mtaalumu huyu wa Mvua aliamrisha mvua kunyesha na kuilekeza kwa majeshi ya wajerumani huku wapiganaji wake wakishambulia kwa mikuki na mishale ya uchungu, Ilikuwa ni vita ngumu iliyowashangaza wajerumani na kuita Miujiza ya kiafrika .
Mnamo mwaka 1901 Wajerumani walianza kuingia Turuland , Iramba na Isanzu wakitokea boma la Kilimatinde - Manyoni walikoweka kambi ya kimkakati .
Mwaka 1902 Jeshi la wajerumani wakitumia farasi , Huko Iambi lilivamiwa na wapiganaji wa kienyeji na kupewa kichapo kikali sana baada ya KITENTEMI kuituma mvua iliyowavuruga wajerumani na kuona Giza tupu hivyo kupewa kipigo cha uhakika na kukimbia eneo la Pambano kwa amri ya Sajenti Zahn . Maafisa wawili wa jeshi la kijerumani waliuawa na wapiganaji wa kinyiramba na wanyisanzu .
Inaelezwa wajerumani walikimbia kama watoto pamoja na bunduki zao kutoka Iambi na kurudi Mkalama ambapo Sajenti Zahn ilibidi aombe msaada kutoka ngome yao kubwa ya Mpwapwa na kikosi kilitumwa haraka kuja eneo la vita , awamu hii wajerumani walipata ahueni baada ya kufanikiwa kumsaka na kumkamata KITENTEMI mtaalamu wa mvua na akachukuliwa toka Mkalama kupelekwa Kilimatinde-Manyoni na kunyongwa . kifo cha KITENTEMI ilikuwa ni pigo kwa wapiganaji wenyeji ambapo Pambano la pili waliweza kuuawa wengi sana na kushindwa na wajerumani wakapata nguvu ya kuweka kambi Mkalama na kujenga boma lao lililoanza kujengwa 1902 na kukamilika 1910 .
Kabla ya vita na wajerumani KITENTEMI anatajwa pia kushiriki vita kati ya Wanyisanzu na wamasai waliovamia Mkalama kwa ajili ya kuiba na kupora ng'ombe ambapo alituma mvua ya mawe umbali wa mita 500 na kuwasambaratisha wamasai .
Inaelezwa mtoto wa Dada yake KITENTEMI aliyeitwa KALI na mdogo wake wa kike aliyeitwa NYAMATALU alimaarufu ANYAMPANDA walirithi Sayansi ya kutengeneza mvua ila haikuwa na nguvu na baadaye walihama kutoka Mkalama na kuhamia eneo la WAHADZABE upande wa kaskazini mwa Mkalama na hali ya amani ilitulia na vita viliisha .
Baadae KALI na NYAMATALU walirudi Mkalama ambapo KALI alitawazwa na wajerumani kuwa Chief au MTEMI KALI wa Mkalama na NYAMATALU alipewa kazi kwenye ofisi za wakoloni .
Chief KALI alifariki mwaka 1927 akiwa Mzee sana na nafasi hiyo kuchukuliwa na Mtemi SAGILU (Sakilu) au ASUMANI mpaka alipofariki mwaka 1939 na kumwachia Mtemi Gunda .
Mwandishi wa makala hii ni ndugu ALFRED RINGI ni mwanahistoria aliyemua kufuatilia na kuwaibua mashujaa wetu waliosahaulika ili waweze kutambuliwa na kuwa sehemu ya Historia ya nchi yetu . Taarifa nyingi zilizofichwa zipo kwenye makumbusho ya Wakoloni wetu huko Ujerumani .habari ni kwa msaada wa Maandiko na Simulizi za Wazee .( Oral and Written sources )
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni