Jumapili, 29 Desemba 2019

MFAHAMU MWANAUME SHUJAA WA SINGIDA ALIYETUMIA MVUA KUPAMBANA NA WAJERUMANI

MFAHAMU  MWANAUME SHUJAA WA SINGIDA ALIYETUMIA MVUA KUPAMBANA NA WAJERUMANI

-Ni KITENTEMI wa Isanzu- Mkalama
-Aliweza kutengeneza mvua wakati wowote  na kuituma kwa Maadui zake wajerumani na kuielekeza anavyotaka .

KITENTEMI mwanaume shujaa wa Singida aliyepambana vita kali na wajerumani walipojaribu kukanyaga ardhi ya Mkalama ambapo mtaalumu huyu wa Mvua aliamrisha mvua kunyesha na kuilekeza kwa majeshi ya wajerumani huku wapiganaji wake wakishambulia kwa mikuki na mishale ya uchungu, Ilikuwa ni vita ngumu iliyowashangaza wajerumani na kuita Miujiza ya kiafrika .

Mnamo mwaka 1901 Wajerumani walianza kuingia Turuland , Iramba na Isanzu wakitokea boma la Kilimatinde - Manyoni walikoweka kambi ya kimkakati .

Mwaka 1902 Jeshi la wajerumani wakitumia farasi , Huko Iambi  lilivamiwa na wapiganaji wa kienyeji na kupewa kichapo kikali sana baada ya KITENTEMI kuituma mvua iliyowavuruga wajerumani na kuona Giza tupu hivyo kupewa kipigo cha uhakika na kukimbia eneo la Pambano kwa amri ya Sajenti Zahn . Maafisa wawili wa jeshi la kijerumani waliuawa na wapiganaji wa kinyiramba na wanyisanzu .

Inaelezwa wajerumani walikimbia kama watoto pamoja na bunduki zao kutoka Iambi na kurudi Mkalama ambapo Sajenti Zahn ilibidi aombe msaada kutoka ngome yao kubwa ya Mpwapwa na kikosi kilitumwa haraka kuja eneo la vita , awamu hii wajerumani walipata ahueni baada ya kufanikiwa kumsaka na kumkamata KITENTEMI mtaalamu wa mvua na akachukuliwa toka Mkalama kupelekwa Kilimatinde-Manyoni  na kunyongwa . kifo cha KITENTEMI ilikuwa ni pigo kwa wapiganaji wenyeji ambapo Pambano la pili waliweza kuuawa wengi sana na kushindwa na wajerumani wakapata nguvu ya kuweka kambi Mkalama na kujenga boma lao lililoanza kujengwa 1902 na kukamilika 1910 .

Kabla ya vita na wajerumani KITENTEMI anatajwa pia kushiriki vita kati ya Wanyisanzu na wamasai waliovamia Mkalama kwa ajili ya kuiba na kupora ng'ombe ambapo alituma mvua ya mawe umbali wa  mita 500 na kuwasambaratisha wamasai .

Inaelezwa mtoto wa Dada yake KITENTEMI aliyeitwa KALI na mdogo wake wa kike aliyeitwa NYAMATALU  alimaarufu ANYAMPANDA walirithi Sayansi ya kutengeneza mvua ila haikuwa na nguvu na baadaye walihama kutoka Mkalama na kuhamia eneo la WAHADZABE upande wa kaskazini mwa Mkalama na hali ya amani ilitulia na vita viliisha .

Baadae KALI na NYAMATALU walirudi Mkalama ambapo KALI alitawazwa na wajerumani kuwa Chief au MTEMI KALI wa Mkalama na NYAMATALU alipewa kazi kwenye ofisi za wakoloni .

Chief KALI alifariki mwaka 1927 akiwa Mzee sana na nafasi hiyo kuchukuliwa na Mtemi  SAGILU (Sakilu) au ASUMANI mpaka alipofariki mwaka 1939 na kumwachia Mtemi Gunda .

Mwandishi wa makala hii ni ndugu ALFRED RINGI ni mwanahistoria aliyemua kufuatilia na kuwaibua mashujaa wetu waliosahaulika ili waweze kutambuliwa na kuwa sehemu ya Historia ya nchi yetu . Taarifa nyingi zilizofichwa zipo kwenye makumbusho ya Wakoloni wetu huko Ujerumani  .habari ni kwa msaada wa Maandiko na Simulizi za Wazee .( Oral and Written sources )

Ijumaa, 6 Desemba 2019

MKAPA ALIKUWA KIJANA WA NYERERE

MKAPA ALIKUWA KIJANA WA NYERERE

Nimemaliza kusoma kitabu cha mzee Mkapa na nilichojifunza ni kuwa Mkapa alitengenezwa na Mwalimu Nyerere.

Mkapa alianza kufundishwa na Nyerere St. Francis College Pugu katika mwaka wa mwisho wa Mwalimu kuwa pale ni wakati Mkapa alikuwa amejiunga hapo mwaka 1955 alimfundisha Kiingereza kwa muda mfupi kabla ya kujuliuzulu mwezi Machi 1955.

Baada ya kumaliza Makerere Mkapa alitaka kujiunga na wizara ya mambo ya nje lakini kwa kuwa hakuwa na uzoefu ilibidi aingie kwanza Serikalini na alipelekwa kuwa District  Officer Cadet  Dodoma Aprili 1962.

Agosti 1962 alikwenda Columbia University ili kusoma kozi ya Foreign Relations. Kozi ambayo ilimfanya kufanya kazi Wizara ya Mambo ya nje na Mwaka 1963 Alianza kazi Mambo ya nje wakati huo waziri akiwa Oscar Kambona akiwa kama Foreign Services Officer grade 3. Na hapo ndipo alipoanza kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu kazi yake hasa ikiwa ni kuandika notes wakati Mwalimu au Kambona alipotembelewa na wageni kutoka nje. Pia alifanya kazi ya kusoma habari Radio Tanzania kutokana na umahiri wake wa kujua vizuri Kiingereza.

Anasema Jioni mmoja baada ya kusoma habari aliambiwa kuwa alikuwa akiitwa na Mwalimu Msasani na alipofika Mwalimu alimwambia kuwa alitaka awe Mhariri wa gazeti la chama The Nationalist. Baada ya Mkapa kusema kuwa hakuna tabu isipokuwa hakuwa na uzoefu na magazeti Mwalimu alimwambia kuwa atamfanyia mpango wa kwenda UK kujifunza.

Baada ya kutoka UK aliajiriwa kama Mhariri wa The Nationalist na Mwalimu mwenyewe akiwa Mhariri Mkuu ( Editor in chief). Kupitia gazeti hilo Mwalimu akisaidiana  na Mkapa waliweza kueneza Siasaa na Propaganda za chama cha TANU. Pia Nationalist na The Standard yaliunganishwa na kuwa Daily News ambalo Mkapa alikuwa Mhariri wake Mkuu wa kwanza Aprili 1972.

Baadae mwaka huo wa 1972 Mwalimu alimteua kuwa Mwandishi wake binafsi na anasema ilibidi amfuate Butiama kuanza kazi kwa kuwa alikuwa likizo huko wakati anafanya uteuzi kazi ambayo alifanya kwa muda wa miaka miwili. Katika kipindi hicho alifanya kazi kwa karibu na katibu myeka wa Rais Joan Wickens na alikuwa akiambatana na Mwalimu katika Mikutano hasa ile ya Nchi zilizokuwa Mstari wa Mbele wa Ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Mwaka 1974 Mwalimu alimwambia aanzishe Shirika la Habari la Taifa( SHIHATA) na alikuwa Mtendaji wake Mkuu kwa miaka miwili.

Aliteuliwa kuwa balozi Nigeria mwezi Oktoba 1976  na baadae kuitwa kuwa Waziri wa mambo ya nje Februali 1977. Anasema huo ndio ilikuwa mwanzo wa safari yake ya Kisiasa. Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Mbunge kupitia Ushirika na Mwaka 1985 alisimama kugombea Ubunge wa jimbo la Nanyumbu na pia Mwaka 1990 alitetea kiti chake. Mwaka 1995 hakugombea.

Anasema Mwalimu alikuwa akimtegemea sana na kwamba kati ya 1976 hadi 1985 wakati Mwalimu anastaafu alifanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo  Nigeria1976, Canada 1982, USA 1883-84, alikuwa Waziri wa nje mara mbili 1977-1980 na pia 1984 -1990 pia kama waziri wa Habari na Utamaduni 1980-1982.

Baada ya Mwinyi  aliendelea kuwa waziri wa Mambo ya Nje  kabla ya kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji 1990-1992 na Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya juu 1992-1995  . Anasema hamahama hiyo ilikuwa ngumu kwa familia yake hasa kuhamisha watoto shule mara kwa mara. Hata hivyo anamshukuru Mke wake Anna ambaye alikuwa muelewa. Kuna kipindi anasema ilibidi watoto wao wabaki Marekani ili kuweza kukamilisha masomo yao.

Mkapa anaelezea kuwa baada ya kipindi cha Mwìnyi kufikia ukingoni aliona baadhi ya watu waliokuwa wametangaza Nia kuwa hawakutosha na kwamba angeweza mwenyewe kupokea kijiti. Baada ya kushauriana na mkewe na kuungwa mkono ilibidi amtumie ujumbe Mwalimu akimueleza kuwa anataka kugombea urais, na baadae alikutana naye na kumueleza   sababu zake za kufanya hivyo:-

Mosi, kuwa Mahusiano ya chama na Serikali hayakuwa mazuri na pia Vyama vya Ushirika ambavyo Mwalimu alikuwa amavipigania na vilikuwa imara wakati kudai uhuru na wakati wa utawala wake vilikuwa vikilegalega, kwamba viongozi wa Ushirika walikuwa wamejifanya wamiliki na wezi

Pili, kuwa Vyama vya Wafanyakazi ambavyo vilikuwa imara na watu kama Rashid Kawawa wakiwa Wawakilisha wa Trade Unions waliendesha harakati za kudai Uhuru, lakini Kulikuwa na migogoro na Chama cha Wafanyakazi walikuwa wametishia kuitisha mgomo.

Tatu, alimwambia kuwa Mwalimu alikuwa ameacha uhusiano mzuri na nchi za Nordic ambao walikuwa wafadhili lakini kwa wakati huo walikuwa wameacha kutoa misaada.

Nne, alisema kuwa ingawa Mwalimu alikuwa hapendi IMF na Benki ya Dunia lakini walikuwa wameanza kuonesha namna ya kusaidia katika kuinua Uchumi, hata hivyo walikuwa pia hawana tena imani na Serikali.

Mwisho, Mkapa alisema alikuwa ameona watangaza nia wengine na kuona walikuwa hawatoshi na kwamba nafsi ingemshitaki asingejaribu kurusha karata yake.

Mwalimu baada ya kumsikiliza Mkapa alimwambia kuwa japo hakumpigia chapuo na kuwa kulikuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa akimfikiria lakini mtu huyo alitaka kama vile kubembelezwa. Basi akasema atamuumga mkono. Hivyo ndivyo Mkapa alivyotangaza Nia baada ya hapo, na kufanikiwa kuupata Urais.

Mkapa pia anaongelea Ubinafsishaji na jinsi Mwalimu  hakupenda hasa uuzaji wa NBC. Anatetea kuwa Mwalimu baada ya kueleweshwa alielewa na hakuwa na neno na Ubinafsishaji wa NBC. Hasa baada ya kuunda NMB, Anaendelea kusema kuwa Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma ulikuwa wa lazima na kuwa hakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuyapiga mnada wa jumla

Mwalimu pia alifurahia misamaha ya madeni kutoka Paris Club ambayo ilanzishwa wakati wa Mkapa na anasema wakati akiwa kitandani Katika Hospitali huko London Mkapa alimpigia simu na kumwambia nchi ilivyosamehewa baadhi ya madeni ,anasema ndio ilikuwa simu ya mwisho kwa Mwalimu kabla ya kuaga dunia na kwamba alifurahi sana.

Mkapa anasema katika kutekeleza malengo aliyokuwa amesema angeyarekebisha wakati akiomba ridhaa ya Mwalimu aweze kugombea ni kuwa:- Aliunda time ya Warioba kuhusu mianya ya rushwa na baadae akaunda PCB,
Pia aliunda Tume ya Makinda na Kahama kuhusu Ushirika, na baadae alimteua Sir. George Kahama kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko japo anasikitika kuwa baadae Kikwete aliivunja hiyo Wizara na Ushirika ikawa Idara kwenye Wizara ya Kilimo

Kuhusu Mahusiano ya Kimataifa pamoja na IMF na Benki ya Dunia anasema alifanya vizuri sana na kuwa alikuwa na Mahusiano ya Karibu ya kikazi na Viongozi wa Taasisi hizo kiasi kwamba mwaka 2001 Horst Kohler na James Wolfensohn walifanya mkutano na wakuu wa nchi za ukanda huu hapa Tanzania,
Pia waliendelea kufadhili miradi mkubwa kama barabara.

Mkapa alifanikisha kuunda Mamlaka za Serikali kama TRA, Wakala za Serikali kama TANROADS, Taasisi za udhibiti, Taasisi na mifuko ya kuinua Wananchi kama MKUKUTA, MKURABITA nk.

Pamoja na mafanikio Mkapa anasema kuna baadhi ya mambo hayakwenda vizuri katika utawala wake ikiwemo mauaji ya Zanzibar, pamoja na wizi wa EPA.

Mzee Mkapa ameandika, Wazee wengine nao waige.

Sylvanus Kamugisha
Dar es salaam.
6, Desemba, 2019.